Mark 15

Isa Mbele Ya Pilato

(Mathayo 27:1-14; Luka 23:1-5; Yohana 18:28-38)

1 aAsubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Isa, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.

2 bPilato akamuuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”

Isa akajibu, “Wewe umesema.”

3Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. 4 cPilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”

5 dLakini Isa hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.

Pilato Amtoa Isa Asulubiwe

(Mathayo 27:15-26; Luka 23:13-25; Yohana 18:39–19:16)

6 eIlikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka. 7Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. 8Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.

9Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?” 10 fKwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Isa mikononi mwake kwa ajili ya wivu. 11 gLakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.

12Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”

13Wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe!”

14Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulubishe!”

15 hPilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Isa achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.

Askari Wamdhihaki Isa

(Mathayo 27:27-31; Yohana 19:2-3)

16 iAskari wakampeleka Isa hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio,
Praitorio maana yake ni makao makuu ya mtawala; ni jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu.
wakakusanya kikosi kizima cha askari.
17Wakamvalisha Isa joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani. 18Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 19Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki. 20 kWalipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.

Kusulubiwa Kwa Isa

(Mathayo 27:32-44; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)

21 lMtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Iskanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 22 mKisha wakampeleka Isa mpaka mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 23 nNao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa. 24 oBasi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.

25 pIlikuwa yapata saa tatu asubuhi walipomsulubisha. 26 qTangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: “Mfalme wa Wayahudi.” 27 rPamoja naye walisulubiwa wanyang’anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [ 28 sNayo maandiko yakatimizwa, yale yasemayo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.]” 29 tWatu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”

31 uVivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 vBasi huyu Al-Masihi,
Al-Masihi maana yake ni Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.
huyu Mfalme wa Israeli, ashuke sasa kutoka msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.

Kifo Cha Isa Msalabani

(Mathayo 27:45-56; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)

33 xIlipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa. 34 yMnamo saa tisa, Isa akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

35Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni anamwita Ilya.”

36 zMtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”

37 aaKisha Isa akatoa sauti kuu, akakata roho.

38 abPazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini. 39 acBasi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Isa aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

40 adWalikuwepo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome. 41 aeHawa walifuatana na Isa na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwepo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu.

Maziko Ya Isa

(Mathayo 27:57-61; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)

42 afIlipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi, yaani siku moja kabla ya Sabato, 43 agYusufu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na ambaye alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Isa. 44Pilato alikuwa akijiuliza kama Isa alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Isa alikuwa amekwisha kufa. 45 ahBaada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yusufu ruhusa ya kuuchukua huo mwili. 46 aiHivyo Yusufu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi. 47Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.
Copyright information for SwhKC